islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUWAKUMBUSHA WATU DALILI ZA MWENYEZI MUNGU KATIKA VIUMBE


9755
wasifu
mwenyezi mungu s.w. ndie peke anae stahiki kuabudiwa kwani yeye ndie mumba wakila kitu,katika dunai hii ameumba mbingu na ardhi, jua na mwezi bara na bahari,na wanyama wa bara na baharini,na wote hawa mwenyezi mungu ndie anae waruzuku,na katika viumbe vyote alivyo viumba mwenyezi mungu kuna dalili na ishara yakuwa allah s.a.peke yake ndie anae stahiki kuabudiwa
Khutba ya

Tunamshukuru Allah (Subhaanahu wa Taala) Aliyetupa neema nyingi. Rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Nachukua fursa hii kuwakumbusha watu baadhi ya dalili na alama za kumjua Mungu kupitia viumbe vyake, pia nitabainisha ukubwa wa Mwenyezi Mungu na kwamba Anastahiki kuabudiwa. Vilevile nitagusia suala la watu kumshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetudhalilishia viumbe hivyo, na tutakumbushana kuvitumia viumbe vya Mwenyezi Mungu katika kumuabudu yeye.

Ama baada ya kumtukuza na kumshukuru Allah na pia kumtakia rehma na amani Mtume wetu. Mwenyezi Mungu Ametuamrisha tuamini kwamba yeye yuko. Na Aya zinazozungumzia suala hili ni nyingi sana pia ameumba viumbe vinavyoonesha kwamba yeye yupo.Kwani kupatikana kwa viumbe ni kuonesha kuna aliyeumba.

Enyi ndugu katika imani ! Hakika katika kila kitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ni dalili ya kuonesha kwamba yeye ni mmoja, na ndiye anayestahiki kuabudiwa kwa haki kabisa na haifai kushirikishwa na yoyote wala chochote.

Napenda nizitaje baadhi ya Aya ambazo zimetuamrisha kuzingatia katika ulimwengu.

قال تعالى) : أَوَلَمْ يَنْظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّهُ مِنْ شَيْءٍ وَأَنْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَدِ اقْتَرَبَ أَجَلُهُمْ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ ) [الأعراف: 185]

Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Je hawaangalii ufalme katika mbingu na ardhi na alivyoumba Mwenyezi Mungu katika vitu, na huenda ikiwa umekaribia muda wao wa kuondoka duniani kumalizika. Basi ni maneno gani baada ya Qur’an watayamini}} [Al-Araaf : 185].

وقال) : أَفَلَمْ يَنْظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِنْ فُرُوجٍ6 وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنْبَتْنَا فِيهَا مِنْ كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ7 تَبْصِرَةً وَذِكْرَى لِكُلِّ عَبْدٍ مُنِيبٍ8) [ق6: 8] Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Je hawaangalii mbingu juu yao vipi tuliijenga na kuipamba na kuifanya kuwa haina nyufa. Na ardhi vipi tuliitandaza na kuiweka vigingi (isitikisike) na tukaotesha katika ardhi hiyo kila mimea mizuri hali ya kuwa ni kifumbua macho kwa kila mtu muelekevu}} [Qaaf : 6 - 8].

وقال) : أَفَلَا يَنْظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ 17 وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ 18وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ 19وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ20) [الغاشية17: 20]

Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Je hamwangalii Ngamia vipi ameumbwa, na mbingu vipi zimeinuliwa, na milima vipi imekitwa na ardhi vipi imetandikwa}} [Al-Qaashiyah: 17- 20]. Hizi ni alama ambazo Mola anataka tuzingatie kuumbwa kwake.

Napenda sasa kutaja baadhi ya viumbe vingine vya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Navyo ni vinavyopatikana katika ardhi kama vile; Maji, Madini, Majabali, Mimea aina tofauti tofauti, kwani Mwenyezi Mungu ameidhalilisha ardhi hii kwa manufaa ya wanadamu na wanyama, wanadamu wanailima kwenye ardhi na kupanda mimea ili kujipatia chakula chao, wanatoa maji katika ardhi kwa matumizi yao na pia kuwanywesha wanyama wao. Mwenyezi Mungu amesema

قال تعالى) : وَفِي الْأَرْضِ آَيَاتٌ لِلْمُوقِنِينَ )[الذاريات: 20]

Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Na katika ardhi kuna alama nyingi kwa wenye yakini}}. Tukiangalia mbinguni kuna nyota nyingi, jua, mwezi na sayari nyinginezo. Vilevile mbinguni kuna viumbe vya Mwenyezi Mungu ambao ni Malaika wanaotekeleza kazi alizowapa Mola aliyetukuka.

Na katika alama nyingine za kumjua Mwenyezi Mungu ni usiku na mchana. Mchana ni wakutafuta maisha na riziki na usiku ni kupumzika.

قال تعالى) وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا 10وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا ) [النبأ10: 11]

.

Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Na tumeufanya usiku ni nguo na tukaufanya mchana ni wa kutafuta maisha}}. Na katika alama hizi mbili za usiku na mchana amewafanyia watu mchana kwenda katika ardhi ya Allah na kutafuta fadhila zake na katika kutafuta fadhila hizo atazidi kubainikiwa mwanaadamu na kuzifahamu alama nyingine za Mwenyezi Mungu. Na katika usiku ni wakati wa kujipumzisha baada ya uchovu wa mchana katika hali ya kutafuta riziki na kutafuta maisha.

Tukigusia zaidi alama za Allah ni wanyama wengi wakubwa kwa wadogo na katika wadogo kuna wadogo zaidi, kuna wengine ametufanyia kuwatumia katika kazi zetu za kila siku, kama kubeba mizigo na kutupeleka sehemu nyingine Na dalili ya alama za Mwenyezi Mungu ni kuumbwa kwetu kwani kuna mazingatio makubwa sana.

قال تعالى: (وَفِي أَنْفُسِكُمْ أَفَلَا تُبْصِرُونَ ) [الذاريات: 21] Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema:{{Na je katika nafsi zenu basi hamuoni}}. Aya hii inatueleza kuwa katika maumbile yetu wanadamu kuna mazingatio makubwa kumjua Mwenyezi Mungu. Lengo kuu la kumtambua ni kuzingatia katika viumbe vyako ni kumjua yeye ili kumthamini, kwani tukimthamini tutamuabudu haki ya kumuabudu na hilo ndio lengo kuu la kuumbwa majini na binadamu.

قال تعالى : ((وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ) [الذاريات: 56 Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema: {{Na sikuumba na majini na binaadamu isipokuwa waniabudu}}. Napenda kusema kwamba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ndiye aliyeumba ulimwengu wote na viumbe vyote bila usaidizi wa mtu yoyote na yeye ndiye anayeupeleka ulimwengu huu. Kwa hivyo, Yeye ndiye anayestahiki ibada kwa sababu hakuna yoyote aliyemsaidia katika uumbaji. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa kuumba na anaupeleka ulimwengu aliomba anavyotaka na wala haulizwi kwa analofanya bali viumbe ndio watakaoulizwa katika vitendo vyao.

Ndugu katika imani! Jueni ya kwamba viumbe vyote ambavyo vinapatikana ulimwenguni havijileti vyenyewe bali Mwenyezi Mungu aliyetukuka ndiye aliyeviumba viumbe hivyo.

قال تعالى) : أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ 35أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بَل لَا يُوقِنُونَ) [الطور35: 36]

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema kwenye Kitabu Chake: {{Au mumeumbwa kwa kisichokuwa kitu au nyinyi ndio waumbaji. Au nyinyi ndio mlioumba mbingu na ardhi bali wao hawana yakini}}. Kulingana na Aya hizi zinaonesha kwamba ulimwengu haukujiumba wenyewe na haukuwa kiumbe ambacho hakikumbwa wenyewe na kitu bali lazima tena kuna aliyeumba ulimwengu huu na akasimama kwa jambo lake (huo ulimwengu) naye si mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) hakuna Muumba asiyekuwa Yeye wala Mola asiyekuwa Yeye.

Enyi waumini! Lau mtaambiwa kuna jumba kubwa la ghorofa lililokamilika, halina kasoro yoyote, ya kwamba limejijenga lenyewe mtaamini? Bila shaka hili ni jambo lisilowezekana kabisa. Na lau inasemekana kuwa jumba kubwa la ghorofa limepatikana ghafla mtaamini? sina shaka kwamba mtasema haiwezekani. Kwa hivyo, huu ulimwengu ulio mpana uliokwenda juu na chini. Haiwezekani kabisa kujileta wenyewe na haiwezekani kabisa kujitokeza ghafla bali ni lazima kuna aliyeuleta ulimwengu huu ambaye ni Mjuzi Muweza naye ni Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Tujue ya kwamba hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika kutudhalilishia ardhi na vilivyomo humo. Kwa hivyo, ni lazima kwa kila Muislamu kushukuru neema kubwa za Mwenyezi Mungu Alizotuneemesha Allah Mola wa viumbe vyote. Akipenda Mwenyezi Mungu tutabainisha suala la kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu katika KHUTBA YA PILI.

Enyi waumini! mcheni Allah (Subhaanahu wa Taala) na kumshukuru kwa uongofu aliotupa na aliyotufundisha yale ambayo tulikuwa hatujui katika mambo yaliyo na maslahi katika Dini yetu na kutujuza mambo yasiyofikiwa na akili zetu na ambayo haifungamani na na maslahi yetu hali ya kuwahurumia nyinyi na hamkupewa ilimu isipokuwa kidogo.

Mwenyezi Mungu Aliyetuelimisha vipi alianza kuumba huu ulimwenguni, na ilimu hii huwezi kuipata mpaka kupitia Mtume rehma na amani zimfikie. Na yoyote atakayetaja chochote kuhusu jinsi ya kuumbwa mbingu na ardhi, hakika ni wajibu tulinganishe na mafunzo walio kuja nayo Mitume ikiafikiana na vile walivyotufundisha Mitume, basi itakubaliwa, na ikienda kinyume na maelezo ya Mitume haikubaliwi na ikiwa Mitume hawakubainisha basi sisi itabidi tulinyamazie suala hilo wala haifai kabisa kutia ufundi wetu mpaka itubainikie kuwa ni haki au ni batili.

Khutba ya pili

Kushukuru Neema za Mwenyezi Mungu

Tunamshukuru Mola aliyetukuka. Rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad. Ama baada ya kupeleka shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kumtakia rehma na amani Mtume Muhammad. Tumegusia katika KHUTBA YA KWANZA yanayohusiana na dalili za kumjua Allah katika viumbe vyake, vile vile kubainisha ukubwa wa Mwenyezi Mungu na kustahiki kwake kuabudiwa peke yake, huku tukiangazia kudhalilishwa viumbe mbali mbali kwa maslahi ya wanadamu. Vilevile kulinganiwa watu kutumia viumbe hivi katika kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kumuabudu yeye peke yake. Katika khutba hii ya pili napenda kubainisha shukrani za wanadamu kwa Mwenyezi Mungu kwa neema tofauti tofauti.

Enyi ndugu katika uislamu! Shukrani ni kumsifu aliyekupa neema. Na shukrani kwa mtu inakusanya nguzo tatu muhimu, kiasi kwamba haiitwi shukrani kwa Mwenyezi Mungu mpaka zikamilike, nazo ni:

Mtu kuitambua neema katika moyo wake.

Kuizungumza neema ile kwa ulimi wake.

Kuitumia neema ile katika kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa ufupi kabisa tunaweza kusema kuwa shukurani inafungamana na moyo, ulimi na viungo vya mwanadamu vilivyobakia. Kazi ya moyo ni kuitambua neema ile ya kwamba inatoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na kumpenda Mwenyezi Mungu.

Na kazi ya ulimi ni kuitaja neema ile na kumsifu Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo na viungo vilivyosalia kazi yake ni kuvitumia katika kufanya maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Tusisahau ya kwamba kuna faida anayoipata mwenye kumshukuru Mola na faida hiyo ni radhi zake Allah (Subhaanahu wa Taala).

قال تعالى) : وَاللَّهُ أَخْرَجَكُمْ مِنْ بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ لَا تَعْلَمُونَ شَيْئًا وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ )[النحل: 78]

Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Mwenyezi Mungu Amewatoa katika matumbo ya mama zenu hali ya kuwa hamjui chochote akawajaalia masikio, macho na moyo ili mumshukuru yeye}}.

Mtume wetu Muhammad ni mfano mzuri katika kumshukuru Mola (Subhaanahu wa Taala) kwa neema nyingi alizomneemesha yeye na viumbe vyote. Alikuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akiswali mpaka ikivimba miguu yake akaulizwa: Wewe pia wafanya hivi na umeshasamehewa dhambi zako zilizotangulia na zitakazaokuja?. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Je, basi siwi mja mwenye kushukuru]. Na imethibiti kwamba Mu’adh bin Jabal alifundishwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie kukutaja na kukushukuru wewe na kufanya vizuri ibada yako].

Tunajua vyema kila wakati tukumbuke kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutudhalilishia neema nyingi na fadhila zake ili tupate kumuabudu yeye peke yake hana mshirika. Bado anasisitiza katika suala hili la kushukuru neema za Allah kwa kutaja neema za Allah kwa wingi. Anasema Hasan Al Baswariy: ‘ Tajeni neema hizi kwa kwa wingi kwani kufanya hivyo ndio kuzishukuru’. Kwa hakika Mola Amemuamrisha Mtume wake na pia sisi kuzizungumza na kuzitaja neema tulizopewa aliposema (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ) [الضحى: 11]

{{Na ama neema za Mola wako zizungumze}} [Adhuhaa: 11]

Mwisho wa khutba hii, nawausia na kujiusia nafsi yangu kutumia neema za Mwenyezi Mungu vilivyo, kwani utumiaji wa neema vilivyo ni katika kushukuru neema hiyo. Kutumia macho inavyotakiwa ni kuishukuru neema hiyo kwani wako watu hawana neema hiyo ya macho,kutumia ulimi vizuri ni kushukuru neema hiyo ya ulimi. Neema ya mikono na miguu kuzishukuru neema hizi ni kuzitumia katika mambo ya kheri. Maneno haya tuliyoyataja yanatufundisha ya kwamba kila neema ina namna yake ya kuishukuru.Tukimalizia neema ya chakula.

يقول الله تعالى) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا كُلُوا مِنْ طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَاشْكُرُوا لِلَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ) [البقرة: 172] Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema: {{Enyi mulioamini kuleni katika vizuri mulivyoruzukiwa na mumshukuru Allah ambaye mnamuabudu na kumtii}} [Al-Baqara : 172]. Pia Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anasema:

وقال) : فَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاشْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ [النحل: 114]

{{Kuleni katika alivyowaruzuku Allah vilivyo halali vizuri na mushukuru neema za Mwenyezi Mungu ikiwa kweli mnamuabudu}} [Al-Nahal : 144].

Mwisho

Tunamshukuru Mola Aliyetuwezesha kuyazungumza yanayohusiana na baadhi ya alama za kumjua Mungu kupitia viumbe vyake. Pia nimegusia kuhusu ukubwa wa Mungu na kwamba yeye Ndiye anayestahiki kuabudiwa. Vilevile ni kuweza kuchambua suala la watu kumshukuru Mungu aliyetudhalilishia viumbe vyake, na nimewakumbusha katika kutumia neema za Mungu alizotupa kwa kumuabudu yeye.

Mwisho kabisa tunamuomba Mwenyezi Mungu Atujaaliye miongoni mwa wenye kuzishukuru neema zake, na kupata radhi zake, na atujaaliye ni wenye kumcha na kumuabudu yeye mpaka mwisho wa uhai wetu na tuingie katika pepo yake. Na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad.





Vitambulisho: