Kuunga vizazi ni jambo ambalo kwalo Mwenyezi Mungu Anakunjua riziki, Anarefusha umri na Anabarikia mali ya mtu. Kuunga vizazi ni alama ya ukamilifu wa Dini na uzuri wa Uislamu. Na kukata kizazi ni sababu ya kulaaniwa na kuteswa, kupata maangamivu na adhabu, kinafuta baraka na kinarithisha uadui na machukivu.
Shukrani zote ni za Allah (Subhaanahu wa Taala) Aliyetuuisa kumcha yeye peke yake. Na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad aliyesema: [Hatoingia peponi anayewakata jamaa zake].
Enyi waumini! leo tutazungumzia jambo ambalo kwalo Muislamu hukunjuliwa riziki yake na kurefushiwa umri wake nalo ni kuunga jamaa. Na jamaa ya mtu ni mamake, babake, watoto wake na kila ambaye karibu naye kinasaba.
Aya na hadithi zinazozungumzia jambo hili ni nyingi hebu niwatajie baadhi. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema:
قال تعالى) : فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ تَوَلَّيْتُمْ أَنْ تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ) [محمد: 22]
{{Ndiyo yanayotarajiwa kwenu kufisidi katika ardhi na kuwakata jama zenu wakati mkipata ukubwa}}.
Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) miongoni mwa mambo aliyoyalingania mwanzo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuacha ibada za mababu, kuswali, kutoa sadaka, kujihifadhi na uchafu na kuunga jamaa. Na kuunga jamaa ni kuwafanyia wema na kutowaudhi. Pia ni katika kuwafanyia wema kuwapa nasaha, kuwapa ushauri, kuwapenda na kuwapendelea kheri, kuwafanyia uadilifu, kuwaelekeza, kuwafundisha, kuwapa haki zao za lazima na kuvumilia na kusubiri katika maudhi yao.
Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! kuunga jamaa kuna fadhila nyingi na katika fadhila hizo ni kuzidishiwa mtu umri wake na vile vile kukunjuliwa mali yake. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Anayependa kukunjuliwa riziki yake na kurefushiwa umri wake basi aunge jamaa zake]. Na kuunga jamaa kuna daraja kubwa katika Uislamu.
Enyi ndugu Waislamu! Je nyinyi mmesimama katika mipaka ya Mwenyezi Mungu? Je mmezifuata amri zake? Je makemeo yake na makatazo mmeyaepuka? Je mmewafanyia wema jamaa zenu na mnawatembelea?
Enyi mnaotaka kheri duniani na kesho akhera ungeni jamaa zenu na kaeni nao vizuri. Enyi waumini! Je munajua faida za kuwafanyia wema jamaa zenu? Jueni ya kwamba kuna khabari njema za duniani na kesho akhera kwa wenye kuunga jamaa zao. Miongoni mwa faida hizo ni:
Faida za Kuunga Jamaa
Kuunga jamaa ni alama kubwa za ukamilifu wa imani.
Kuunga jamaa ni sababu ya kukunjuliwa mtu katika riziki.
Kuunga jamaa ni sababu ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Nasaha za watu wema juu ya Kuunga Jamaa
Wema waliotangulia wametoa wasia unaoonesha umuhimu wa kuunga jamaa. Amesema ‘Umar ibn Khattwab, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: ‘Jifundisheni nasaba kisha muwafanyie wema jamaa zenu. Amesema ‘Atwaa ibn Abi Rabaa: ‘Kutoa dirham kumpa jamaa yangu inapendeza zaidi kuliko kutoa dirhamu elfu kumpa maskini, mtu akamuuliza: Hata kama jamaa yako ni tajiri? Akasema ‘Atwaa : Ndio, hata kama jamaa yangu ni tajiri’.
Vile vile amesema Said ibn Musayyab Mwenyezi Mungu amrehemu hakika aliwacha Dinari kadhaa: ‘Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe wajua sikuyakusanya mali zangu isipokuwa kwa ajili ya kuhifadhi Dini yangu,. Hana kheri asiyekusanya mali yake kulipa deni lake na kuwafanyia wema jamaa zake”.
Kutahadharishwa Kuwafanyia Ubaya Jamaa Zako
Shukrani za dhati zinamstahiki Mola wa viumbe wote Aliyetuamrisha kuunga jamaa zetu na Akatukataza kuwafanyia ubaya. Na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad ambaye ni kiigizo chema katika kuunga jamaa zake.
Ama baada ya hayo: Enyi waumini kama ambavyo kuunga jamaa kuna ujira mkubwa. Vilevile kuwavunja jamaa kuna hasara na madhambi makubwa Napenda nikutajie baadhi ya hasara hizo:
Hasara ya Kuwafanyia Ubaya Jamaa
Kuwakata jamaa ni miongoni mwa sababu za mtu kutoingia peponi. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema ya kwamba: [Hatoingia peponi mtu anayewakata jamaa zake].
Na katika hasara za kukata jamaa ni kupata laana ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema kwenye Kitabu chake kitukufu: Ndiyo yanayotarajiwa kwenu kuleta uharibifu katika ardhi na kuwakata jamaa zenu wakati mukipata ukubwa. Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu Akawatia uziwi masikio yao na akayapofua macho yao.
Na kosa kubwa kabisa ni mtu kuwakata wazazi wake wawili kisha akawakata walio karibu zaidi naye. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Je siwajulishi dhambi ambalo ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa? Wakasema maswahaba: Tujulishe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwakata wazazi wawili].
Pia miongoni mwa hasara za kukata jamaa ni kufanyiwa haraka mtu kuadhibiwa hapa duniani kabla kuadhibiwa kesho akhera. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hakuna kosa ambalo Mwenyezi Mungu analiharakisha zaidi adhabu yake kwa mwenye kulifanya duniani pamoja na kuwekewa adhabu nyingine akhera kuliko kuwakata jamaa na kufanya maasia].
Enyi ndugu katika imani! Hakika jamaa wana daraja tofauti tofauti katika kuishi nao:-
Jamaa wenye kushikamana na Dini na jamaa aina hii hufanyiwa wema kwa kule kushikamana kwao na Dini.
Jamaa ambao wazushi ni katika Dini na wenye kufanya maovu. Na hawa wamegawanyika vigawanyo viwili:-
Wanaotangaza bidaa na uzushi wao na maovu yao tena wanalingania kwenye uovu huo. Jamaa hao hupigwa vita kabisa kwa ajili ya kushikamana kwao na uovu. Inafaa kuwaonesha uso wa bashasha, lakini haifai kuwa nyoyo zetu haziko radhi nao moyoni kwa ule uovu wao. Ushahidi wa hilo ni kwamba Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Alimwonesha bashasha ‘Uyaina ibn Hiswhiy aliyekuwa mtu muovu kabisa. Alipokuwa akibisha kwake huku akisema : Ni ndugu muovu katika jamii. Alipoingia Mtume alizungumza naye vizuri akasema: Hakika tunawaonesha uso wa bashasha watu (waovu) na huku nyoyo zetu zawalaani].
Jamaa wafichao bidaa na vitendo vyao viovu, jamaa aina hii hufanyiwa muamala wa Waislamu wasiojulikana maovu yao.
Jamaa walio makafiri na wanafiki na jamaa aina hii wamegawanyika mara mbili:-
Jamaa wanaoupiga vita Uislamu jamaa aina hii hukatwa na hauwaungwi kwa ajili ya kuogopwa shari lao.
Jamaa wasiopiga vita Dini yetu ya uislamu jamaa aina hii hufanyiwa wema kwa njia zifuatazo:-
Kuwalingania katika Uislamu kwa njia nzuri.
Kuwaombea dua Mwenyezi Mungu Awaongoze katika Uislamu.
Kuwasaidia wanapokuwa na shida na kuwafanyia wema kuwavutia katika Uislamu.
Mwisho
Tunawahimiza Waislamu popote waliopo kushikamana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu hasa suala zima la kuwatendea wema jamaa. Tufahamu ya kuwa Jamaa ni msingi wa jamii ya kiislamu, na jamaa ikishikamana, jamii itashikamana. Tukifanya hivyo, tutaweza kujenga umma mmoja wa kiislamu, na kuanzishwa kwa serikali ya kiislamu. Bila ya kujenga msingi wa jamaa moja, hatuwezi kufikia lengo la kurejesha Ukhalifa katika ardhi. Ni jukumu la kila Muislamu kufanya bidii kuunga jamaa yake na kujenga jamii ya kiislamu iliyoshikamana. Tunamuomba Allah atuwezeshe kurejesha umoja wa kiislamu na Atujaalie ni wenye kuwatendea wema jamaa zetu na tufaulu kuipata pepo yake.