islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


UTWAHARA WA MGONJWA KATIKA UISLAMU


8422
wasifu
Huruma ni sifa ya Mwenyezimngu Aliyetukuka Aliyosifika nayo na Akaitia kwenye moyo wa Mtume Wake, na Akaijaalia ni alama iliyo wazi katika Sheria Zake Alizoziwka. Na mwenye kuzitaamaki hukumu za Sheria zote, atapata rehema ambayo zitadhihiri sura zake na maana yake. Na mwenye kutaamali maisha ya Mtume Muhammad, ataona kuwa huruma imejikita katika tabia yake.
Khutba ya

Ewe Muislamu, Mola amekuumba na atakupa mitihani, basi utakapopata mitihani hiyo usisahau ibada Yake kama kawaida, tena haswa ibada ya swala.

Utwahara wa Mgonjwa na Swala zake

Baada ya himidi na swala na salamu, Enyi watu, muogopeni Mwenyezi Mungu kisawa sawa. Ewe muislamu, ujuwe Mola alituafikia, mimi na wewe tupate kheri ya Uislamu na bila shaka, maadamu ni Waislamu tutapata mitihani kila aina, ya siri na ya dhahiri ili tumtambue, tumshukuru na kusubiri. Na ndio Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) akasema katika maana ya Aya:

يقول الله جلّ وعلا: (وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّى نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنْكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ) [محمد: 31]

.

{{Hakika tutawaonja mpaka tujue waumini wa kweli na wavumilivu miongoni mwenu}}.

Mwanafunzi wa Mtume, Suhaib Ar-Rumii amesema kwamba Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Ajabu ni ya huyu Muislamu, kwa kuwa kila jambo lake ni nzuri. Akipata la kumfurahisha atashukuru na ni kheri kwake, na akipata la kumuudhi atavumilia na ni kheri kwake]. Amepokea hadithi hii Muslim. Kwa hivyo, Muislamu atavumilia na ataridhike alivyomuahidi Mola.

Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema katika maana ya Aya:

قال تعالى) : إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُمْ بِغَيْرِ حِسَابٍ ) [الزمر: 10]

{{Hakika watalipwa wavumilivu malipo mengi pasi kuwa na hesabu}}. Bishara njema kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala) kwa wenye kuvumilia na kusubiri. Amaesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ155 الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ156 أُولَئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ) [البقرة155: 157]

{{Tena wape habari njema wavumilivu, ambao wakipatwa na msiba husema, hakika sisi ni wa Allah kwa hakika sisi kwake yeye tutarejea, hao watapata msamaha na rehma kutoka kwa Mola wao na wao ndio waongofu}}.

 

Na katika Hadithi, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anasema: [Muumini akikumbwa na shida yoyote, huzuni na kadhalika, hata kudungwa na mwiba, yote humfutia madhambi].

Mja hapendelei Mitihani

Mja hatakikani apende mitihani wala apatikane na shida yoyote kwa sababu hajui ataweza kuvumilia au la. Kwa hivyo Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimjibu Ammi yake ‘Abbas alipomuomba amuombee dua, Mtume akamwambia: [Ewe Ami, omba Mungu akupe afya, na akamkariria hilo]. Habari nyingine kutoka kwa babake Mu’adh Ibn Rafai anasema kuwa alisimama Abu Bakar Swiddiq akihutubu kisha akalia akasema: Mtume alisimama katika mimbari hii akahutubu kisha akalia akawa anatuambia: [Muombeni Mungu msamaha na afya kwani hakuna kitu muhimu baada ya imani na yakini isipokuwa ni afya na kila wakati mja atake msamaha na Mola ampe afya].

Ewe Muislamu, ukiwa na afya yako jikurubishe kwa Mwenyezi Mungu vile utakavyoweza na siku ukiwa mgonjwa akashindwa kufanya kama ulivyokuwa ukifanya basi fanya utakavyoweza na Mola atakulipa kama ulivyokuwa ukifanya ulipokuwa mzima, kama vile swala ya mgonjwa na swala ya msafiri.

Umuhimu wa Swala na Uwajibu wa Kuitunza

Enyi waja wa Allah, Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) amesema katika maana ya Aya: “Hakika swala ni lazima kwa muumini kwa wakati niliopanga” na Mtume akawaeleza kwa uwazi zaidi. Ewe Muislamu hakika tabia ya muumini ni kuifanya umuhimu wa swala kwa wakati vile alivyotufundisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Allah (Subhaanahu wa Taala) Anasema:

قال تعالى: (الَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَاتِهِمْ دَائِمُونَ ) [المعارج: 23]

{{Waja wema ni wale wanaofululiza swala zao pasina kuacha}}. Kwa hivyo, swala iwe ndani ya moyo wa muumini, afuzu nayo na ajisikie nayo, na maadamu akili yake ni nzima basi anaamrishwa kuswali kwa vyovyote vile kama Mola alivyomuamrisha Mtume Issa Ibn Mariam, alimuamrisha kuswali na kutoa Zaka maadamu yuko hai.

Jitahadhari na Wenye kudharau Swala.

Ewe Muislamu, baadhi yetu wanaacha swala sio kwa sababu ya uvivu, bali dunia imeingia ndani ya nyoyo zao mpaka wakati ukapita, tena sana. Ikiwa mtu ni mgonjwa ni ajitahidi kuswali kwa hali yoyote mpaka apoe maradhi, na akipoa ataswali kama mwenye afya yake.

Utwahara kwenye Swala ni lazima.

Hili ni jambo lililo maarufu na ya kuwa utwahara kwenye swala ni lazima, katika nguo utakazoswalia na mwili wako wakati ule unaswali na mahali unaposimama kuswali. Mola (Subhaanahu wa Taala) Anasema katika maana ya Aya:

قال تعالى: (وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ) [المدثر: 4[

{{Na nguo zako, ewe Muhammad, uzitwahirishe}}.

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akitembelea makaburini akateremshiwa wahyi ya kuwa makaburi mawili kati ya hayo waliomo ndani wanaadhibiwa, kosa la mmoja wao alikuwa hamalizi kujisafisha mkojo na hamalizi mkojo]. Hadith nyingine Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: {{Adhabu wanayoadhibiwa watu wengi ni kuwa hawamalizi mikojo}}, na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema [ Haikubaliwi swala ya mmoja wenu ikiwa hana udhu mpaka atawadhe]. Hivi inamaanisha utwahara wa kila pahali ndio sharia inavyotakikana.

Kujisafisha Magonjwa.

Kujisafisha kwa malengo mawili :-

Kuwa safi mbele ya viumbe wenzako

Kuwa safi mbele ya viumbe wenzako na mbele ya Muumba wako.

Kuwa safi mbele ya viumbe ni kujisafisha choo, mkojo, damu na kadhalika. Na kujisafisha mbele ya Allah ni kujisafisha hivyo na kutawadha au kuoga au kutayammam.

Kutayamam ni pale unapokosa maji au ukiwa mgonjwa. Vilevile yawezekana maji yakawapo lakini ikawa viungo vya udhu vikipata maji utadhurika, ndipo utatayamam, haya yamesemwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika maana ya hadithi ya kuwa: [Ikiwa mnataka kuswali na hamna maji tayamam kwa mchanga kwani huo pia ni wenye kutwaharisha].

Ewe Muislamu mja huenda akakumbwa na maradhi kwenye viungo vya udhu, hapo atafuata moja katika njia mbili:- (1) Atatawadha na pale penye maradhi atapangusa na aende na udhu wake. (2) Ikiwa hivyo vitamdhuru, basi atatayamamu kama kawaida. Swahaba Ibn ‘Abbas alisema: ‘Mwenzetu aliyekuwa na kidonda kwa bahati mbaya alikumbwa na janaba kwa njia ya kuota, wenzetu hawakufahamu wakamueleza aoge, na swahaba akaoga kidonda kikaingia maji maradhi yakamzidi na akafa, tuliporejea mjini, Mtume akapelekewa habari ile, akasema: “Nyinyi mumemuuwa, kama angetayamamu angeendelea kuishi”

Swala ya Mgonjwa.

Ikiwa wewe ni Muislamu na akili yako inafanya kazi, inafahamu na kuelewa, basi swala ni juu yako kwa utakavyoweza, ulazima wake sio kama faradhi nyenginezo, nguzo hiyo iko juu ya mabega yako kwa kila kipindi kikiingia. Ndio utaona Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) mwenyewe na maswahaba na tabiina na waja wema wa kwanza wakitekeleza swala zao kwa afya na maradhi, Anas Ibn Maalik asema: ‘Siku moja nilipanda farasi, nikaanguka chini nikaumia, nikaswali kwa kukaa’.

Swahaba mwengine ‘Imran ibn Huswain amesema kuwa yeye alikuwa mgonjwa wa bawasiri akawa ahisi dhiki kusimama na kukaa. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamuambia: [Swali kwa kusimama, ikiwa huwezi, swali kwa kukaa, ikiwa huwezi swali kwa ubavu. Baadaye Mtume akaondoka, aliporejea akamkuta anaswali kwa kukaa lakini amekalia mto. Mtume akakasirika akauondosha ule mto akautupa kando na akasema: ‘Swali juu ya ardhi ukiweza na kama huwezi swali kwa vyovyote lakini usikose khushui hata kama utaswali ni kwa kuashiria kwa kichwa katika kurukuu na kusujudu, ukirukuu utainamisha kichwa kidogo na ukisujudu ndio sana na iwapo huwezi hivyo, hata ishara ya macho inatosha’. Ama ishara ya kuswali kwa kidole sio sahihi. Haiko kwenye Qur-an, hadithi wala kwenye ilimu. Na wala si vizuri ukiwa unaumwa kidogo ukaswali kwa kukalia kiti, ndipo Misikiti yetu inakaribia kuwa holi kwa viti.

Khutba ya pili

Mgonjwa kuelekea Qibla

Ewe Muislamu, Hapana budi kuelekea Qibla ili swala ikubaliwe, na hii iko wazi kwa wanazuoni wote, lakini mgonjwa akiwa hajiwezi na hakupata mwenye kumsaidia kumuelekeza Qibla na ikiwa kitanda hakikulenga Qibla, ataswali vile alivyojaaliwa, na wakati mwingine mgonjwa huwa ana najisi au hana udhu na hakupata mwenye kumsaidia kwa udhu au kumsafisha uchafu, majeraha yakawa yana damu na usaha, basi ataswali kama alivyojaaliwa. Habari kutoka kwa swahaba mtukufu, Mansuur ibn Makhramah anasimulia ya kuwa aliingia nyumbani mwa ‘Umar ibn Khattwab kwa swala ya asubuhi na ‘Umar alikuwa amedungwa na Abuu lu’lu’ah aliyekuwa katika dini ya kimajusi, lakini ‘Umar alikuwa hajafa bado, majeraha yanamwaga damu na Khalifa akaendelea na swala kama kawaida. Hivi ndivyo waumini wanavyokuwa kipindi cha swala hakiwapiti.

Ni wajibu kwa Msimamizi wa Mgonjwa kumsaidia kumtwahirisha na kumkumbusha swala.

Ewe Muislamu, unaemsimamia mgonjwa nyumbani au hospitalini, Muogope Allah, na ujue ya kuwa swala ni muhimu, umsaidie mgonjwa wako kwa kumsafisha, umkumbushe swala na dhikri na zaidi ikiwa ni wazazi wako, kwani wao unapaswa uwasaidie zaidi kwa kazi hiyo tukufu kama Mola (Subhaanahu wa Taala) Alivyotuamrisha katika maana ya Aya:

قال تعالى : (وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا) [طه: 132]

{{Na uamrishe watu wako swala na uvumilie}}

Ulinganizi kwa Matabibu wamche Mwenyezi Mungu.

Ni sisi Waislamu tuwaelimishe matabibu kuwa Muislamu ni wajibu aswali na kuwa kuswali ndio chakula cha roho. Hao matabibu huwapatia dawa wagonjwa kwa vipindi, nyakati na saa maalumu, tuwakumbushe ilivyo muhimu dawa ya mwili, dawa ya roho ni muhimu zaidi, haifai kujitukuza wala kudharau. Kila kitendo kina wakati wake na Mungu aliyetuumba amesema katika maana ya Aya:

والله يقول: (وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَى وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ( [المائدة: 2] {{Saidianeni katika wema na kumcha Mwenyezi Mungu na wala msisaidiane katika madhambi na uadui}}.

Hukumu ya kukusanya Swala Mbili kwa Wakati Mmoja.

Sheria ya kiislamu imemuhurumia mgonjwa ikamruhusu aswali swala mbili kwa kipindi kimoja, kwa vile ana shida ya ugonjwa, maumivu ya madawa, kutawadha na kumsumbua mwenye kumshughulikia, kwa hivyo atakusanya swala ya Adhuhuri na Alasiri aziswali kipindi cha Adhuhuri au kipindi cha Swala ya Alasiri. Na swala ya Magharibi na Isha aziswali kipindi cha Magharibi, au kipindi cha Ishi. Haya yote ni kwa sababu ya kumhurumia mgonjwa.

Nasaha kwa Waislamu Wote.

Ewe Muislamu, swala iwe ndani ya moyo wako, akili yako roho yako na damu yako, uiswali kwa wakati wake, na sharti zake. Hakuna litakalo kuachisha Swala isipokuwa kufa, ili uingie kwenye pepo ya Firdausi iliyo bora kuliko pepo zote kama vile Mola (Subhaanahu wa Taala) alivyosema katika maana ya Aya:

قال تعالى): وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ 9أُولَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ 10الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ) [المؤمنون: 11]

{{Waja wema ni wale wanaohifadhi Swala zao. Hao wataingia pepo ya Firdausi watakaa humo milele}}. Na hata mkiwa kwenye vita mtaswali kwa kutembea au ikiwa mmepanda vipando au mtaswali kwa zamu, bora kipindi kiingie, mswali kwa hali yoyote ile. Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie sisi tuwe waja wema wenye kutunza swala zetu na hakika yeye kwa kila kitu ni Muweza.

Jueni, Mungu awarehemu, hakika maneno mazuri ni kitabu cha Mungu na uongofu bora ni uongofu wa Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na mambo mabaya zaidi ni yale yaliozuliwa katika Dini, kwani kila lenye kuzuliwa huitwa ni uzushi. Kwa hivyo ni juu yenu mshikamane na Sunnah za Mtume na Maswahaba zake na mumswalie Mtume wenu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kwa kufuata amri ya Mola (Subhaanahu wa Taala) wetu Aliposema katika maana ya Aya:

قال تعالى) : إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ) [الأحزاب: 56]

 

{{Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Mtume, Enyi waumini pia nyinyi mswalieni}}.

Ewe Mwenyezi Mungu, Mswalie na umbariki Mtume Muhammad na watu wake wa kwanza na wa mwisho na uwe radhi na Maswahaba zake na Makhalifa wake na waliokuja baada yao mpaka Qiyama.

Mwisho

Ewe mwanadamu mwenzangu, wewe umeumbwa, hukujiumba, umeletwa hukuletwa, na siku ya kuondoshwa hutajua. Kwa hivyo ni juu yako kumtwii Allah katika saa zote, siku zote, wiki zote, miezi yote, miaka yote mpaka mwisho wa umri wako.

Katika maisha yako, utapata mitihani ya kila aina, magonjwa na kadhalika. Ukipatikana na mtihani wa ugonjwa utaswali kama kawaida na ukishindwa utaswali utakavyoweza, muhimu ni kuwa kipindi cha Swala kisikupite, maadamu akili yako inafanya kazi, swala imekulazimu. Ewe Mwenyezi Mungu, Tupe mitihani mipesi ili tusiepukane na Swala.





Vitambulisho: