islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


HESHIMA YA WANAWAKE KATIKA UISLAMU


13760
wasifu
Mwanamke katika zama za Ujinga alikuwa akidharauliwa na kutwezwa mpaka Uislamu ukaja, ukamheshimu heshima isiyokuwa na mfano. Ukamkomboa kutoka kwenye maonevu ya wakati wa Ujinga na ukamdhaminia haki zake na ukamfanya sawa na mwanamume katika nyajibu nyingi za kidini, na katika malipo mema na mateso. Hajawahi kupata heshima wala takrima vile alivyopata katika sheria ya Kiislamu
Khutba ya

Ndugu katika imani, suala la mwanamke ni suala ambalo liliwashughulisha watu wengi walio pita, na linaendelea kuwashughulisha wengi katika zama zetu hizi. Dini na mila mbalimbali zimezungumzia hali ya mwanamke katika jamii. Wasomi wa elimu na falsafa tafauti wamejaribu kuzungumzia cheo cha mwanamke katika jamii. Lakini kila kundi linajaribu kumzungumzia mwanamke kwa misingi ya kufikia malengo yao. Katika khutba hii tutajaribu kuangazia cheo cha mwanamke katika jamii mbalimbali. Tutaangalia hali ya mwanamke kabla ya kuja Uislamu, na hali yake katika Uislamu, na hali yake katika mataifa ya magharibi.

Hali ya Mwanamke kabla ya kuja Dini ya kiislamu

Alikuwa mwanamke katika zama za ujinga akionekana kama bidhaa ambayo haina thamani. Kila mtu anaweza kumiliki bidhaa hiyo wakati wowote. Wanaume wakioa wanawake bila ya idadi maulumu na kuacha bila ya idadi ya talaka. Mwanamke haruhusiwi kumiliki chochote, hana haki ya kurithi, anaweza kuolewa na zaidi ya mume mmoja. Mwanamke hakuwa na cheo katika jamii ya ujahiliyah, bali alikuwa akionekana ni mtu anayeleta aibu katika jamii. Ikafikia hali hiyo, baadhi ya wanaume kuwazika mabanati wao wakiwa wadogo kuogopea kuleta aibu katika jamii. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anatueleza hali ya mwanamke Akisema:

قال تعالى :(وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُمْ بِالْأُنْثَى ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ 58يَتَوَارَى مِنَ الْقَوْمِ مِنْ سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ أَيُمْسِكُهُ عَلَى هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ) [النحل: 59]

{{Na mmoja katika wao anapopewa khabari ya kuzaliwa mtoto wa kike, unabadilika uso wake huwa mweusi na akajaa sikitiko. Anajificha na watu kwa sababu ya khabari mbaya ile alioambiwa. (anafanya shauri) Je, akae naye juu ya fedheha hiyo, au amfukie udongoni. Ni mbaya mno hukumu yao hiyo}}. Hii ndio hali halisi ya mwanamke kabla ya kuja Dini ya kislamu. Na hali hii ilikuwa sawa katika mataifa yote, sawa taifa la kiarabu na wasiokuwa waarabu.

Hali ya Mwanamke katika Uisalmu

Baada ya mwanamke kuishi katika dhulma kwa muda mrefu, bila ya kupata haki zake. Allah (Subhaanahu wa Taala) Alimtumiliza Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuja kumkomboa mwanamke na dhulma na udhalilifu alikuwa akipata kutoka katika jamii anayo ishi. Dini ya Kiislamu inamtukuza mwanamke na inampa haki zake zote katika jamii. Miongoni mwa haki hizo:-

Mwanamke sawa na mwanamume katika kutekeleza majukumu ya Dini. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى :(مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ) [النحل: 97]

{{Wafanyaji mema, wanaume au wanawake, hali ya kuwa ni Waislamu, tutawahuisha maisha mema, na tutawapa ujira wao mkubwa kabisa}}. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) alimfadhilisha mwanamume kuliko mwanamke katika baadhi ya mambo, kwasababu ya majukumu mazito ya mwanamume katika kusimamia familia.

Mwanamke anastahiki kurithi. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

وقال سبحانه) : لِلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ نَصِيبًا مَفْرُوضًا) [النساء: 7]

{{Wanaume wana sehemu katika mali wanayoacha wazazi wao na jamaa walio karibu. Na wanawake pia wanayo sehemu katika yale waliyaacha wazazi wao na jamaa walio karibu. Sawa yakiwa kidogo au mengi. Ni sehemu zilizofaridhishiwa (na Mwenyezi Mungu)}}.

Mwanamke ana haki ya kuchagua mume wa kumwoa. Hawezi kuolewa bila ya ridhaa yake. Kinyume na zama za jahiliyah, mwanamke alikuwa ni bidhaa na chombo cha starehe kila mtu anakichukuwa kwa thamani ndogo, na kwa lengo la kutekeleza matamanio yake.

Mwanamke ana haki ya kujikomboa kutokana na mume dhalimu. Sheria ya kiislamu imempatia mwanamke haki ya kutoa talaka kwa mwanamume mwenye tabia mbaya, mwenye kumnyima mkewe haki zake.

Haya ni baadhi ya mambo muhimu mabao mwanamke amepewa katika Dini ya kiislamu. Na hii ndio hali halisi ya mwanamke katika Uislamu. Uislamu ulimrejeshea mwanamke hadhi na utukufu wake katika jamii, na ikatambua mchango wake mkubwa katika kuandaa kizazi cha kesho na kulea viongozi wa kusimamia Dini ya kislamu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika Hija: [Mcheni Mwenyezi Mungu katika kuwasimamia wanawake, kwa sababu wao ni wasaidizi wenu]. Mtume anaweka wazi cheo cha mwanamke nacho ni wasaidizi wa wanaume, sio mtumwa au mtumishi kama wanavyomdai watu wengine kwamba uislamu umemfanya mwanamke kuwa ni mtumwa hana haki yoyote katika jamii.

Enyi waja wa Allah, tumcheni Allah na tufanyeni bidii kuwasimamia wake zetu kulingana na alivyo tufundisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Khutba ya pili

Ndugu Waislamu, nawausieni na kujiusia nafsi yangu kumuogopa Allah (Subhaanahu wa Taala), kwani wachaji Mungu ndio wenye kufaulu. Ndugu katika imani, tuangalieni hali ya mwanamke katika nchi zilizoendelea kama wanavyo dai nchi za kikafiri.

Hali ya Mwnamke katika nchi za kikafiri.

Hakika hali ya mwanamke katika nchi hizi ni mbaya sana kushinda hali ya mwanamke katika zama za jahiliyah. Mwanamke amefanywa kuwa ni kivutio cha kila badhaa au biashara kwa kudhihirisha uchi wake bila ya kujali wala kuona haya. Kila tukiangalia runinga, kusoma magazeti, internet tunashuhudia mwanamke ndiye wa kwanza kuonyeshwa hali akiwa uchi kabisa kwa lengo la kuvutia watu katika biashara hiyo. Kwa kweli mwanamke amepokonywa haki zake zote za kimsingi, haki ya kusimamia majukumu ya nyumba, kulea watoto, kuandaa familia juu ya misingi ya tabia njema na maadili mazuri.

Leo mwanamke hana nafasi nyumbani, kazi yake kubwa ni kutoka nje na kwenda kushindana na wanaume, na kudai haki za wanaume katika kazi. Imekuwa hakuna tafauti baina ya mume na mke. Na hili ndilo lengo kubwa la makafiri kumtoa mwanamke nje na kumvunjia heshima yake aliyopewa na Allah (Subhaanahu wa Taala). Na baadhi ya wanawake wa kiislamu wameathirika na tabia mbaya za makafiri. Wakaona haya ndio maendeleo na kuonekana kuwa mtu ameendelea.

Ndugu waumini, ni wajibu wetu kama wazazi kuwatahadharisha wake zetu mabanati wetu na kasumba mbaya za makafiri. Na tujue makafiri hawatokuwa radhi mpaka tufuate mila zao. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى :(وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّهِ هُوَ الْهُدَى وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُمْ بَعْدَ الَّذِي جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ) [البقرة: 120]

{{Hawatukuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila yao. Sema hakika uongozi wa Mwenyezi Mungu ndio uongozi wa sawa. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yale yaliyokufikia ya ujuzi, hutapata msaidizi yoyote wala mlinzi kwa Mwenyezi Mungu}}.

Mwisho

Mwisho ndugu Waislamu, tukumbuke malipo na fadhila atakazopata mwenye kumlea msichana malezi ya kiislamu kisha amuozeshe mume mwenye tabia njema basi huyo amedhaminiwa kuingia peponi. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mwenye kuruzukiwa mabinti watatu, na akasubiri juu ya kuwalea, kwa hakika mtu huyo amewajibika kuingia peponi. Akasema mtu kumuuliza Mtume: vipi ukiwa na wasichana wawili?. Akasema Mtume na wawili pia ni sababu ya kuingia peponi].

Ndugu waumini, angalieni rehma ya Allah juu yetu katika kusimamia majukumu ya Allah kwa kuwalea wasichana kwa maadili mema na tabia njema, Allah atakulipa pepo yake ambayo si rahisi kuingia kila mtu, isipokuwa watakao simamia majukumu hayo.

Tunamuomba Allah atuwafikishe tuweze kutekeleza majukumu yote kwa njia ya kumridhisha yeye peke yake. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu awahifadhi watoto wetu na kila shari ilio dhahiri na siri.





Vitambulisho: