Dini ya Kislamu imepanga sheria ya kila kitu. Na miongoni mwa sheria hizo, ni sheria ya kuishi na kufungamana na watu. Jamii moja inakusanya watu wa ina tofauti – makabila, utamaduni, tabia, Lugha na dini. Muislamu analazimika kuishi na watu wenye mila na dini tofauti kwa tabia mzuri kama tulivyo fundishwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Kila mwanadamu ana haki ya kuishi na ana haki ya kuabudu, kusoma na mengineyo. Lakini haki zote hizi ni lazima Muislamu azifahamu na kuzitekelza kulingana na misingi ya kisheria.
Mizani ya Mwenyezi Mungu katika kupima watu
Tunapozingatia Aya za Qur’an na Hadithi za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) tunaona Mwenyezi Mungu amejaalia utukufu kutokana na dini, taqwa na tabia njema na wala hakujaalia utukufu katika nasaba wala umaarufu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قوله تعالى (إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ) [الحجرات: 13]
{{Hakika mtukufu miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni Yule amchae Mungu zaidi katika nyinyi}}.
Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Mbora wenu anayejifundisha Qur’an na akaifundisha].
Na akasema tena Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mbora wenu anayetarajiwa kheri kutoka kwake na kuaminika na shari zake).
Ameulizwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Nani mbora kati ya watu? Akasema anayemcha Mwenyezi Mungu. Wakasema hatukuulizia swala hilo. Akasema Mtume Yusuf, wakasema hatukuulizia swala hilo, akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Mbora wao katika ujahiliyya ni mbora wao katika uislamu, wakijuwa ubora mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwa kumcha Mwenye na kufanya amali njema].
Mtume wa Mwenyezi Mungu anasawazisha mizani ya watu akasema: [Mwenyezi Mungu haangali sura zenu wala mali zenu lakini huangalia nyoyo zenu na vitendo vyenu].
Amepita mtu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamuuliza mtu aliyekaa nae, rai yako kwa huyu mtu aliyepita? Akasema ni mbora wa watu, akiposa huoa, akanyamaza Mtume wa Mwenyezi Mungu, baada ya hapo akapita mtu mwingine akamuuliza rai yako kuhusu mtu huyu? Akasema huyu ni maskini, huyu ni mbora akiposa huoa, akisema hasikiwi, akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu huyu ni mbora.
Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimuuliza Abu Dhari: [Huoni kuwa na mali nyingi ndio utajiri na kuwa na mali kidogo ni umaskini? Akasema ndio. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akasema utajiri ni utajiri wa moyo na umaskini ni umaskini wa moyo].
Walipozikwa mashahidi alikuwa Mtume akiuliza aliyehifadhi Qur’an zaidi akaashiriwa akawa humtanguliza mtu huyo katika kaburi. Mtume aliuliza pote la watu akamuuliza mzee wao kama amehifadhi Suratul Baqara akasema ndio, akamfanya kuwa kiongozi.
Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amemfanya Ibn Ummi Maktoom ambae ni kipofu kuwa ni kiongozi wa Madina baada kusafiri Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).
Kama alivyomfanya Salmaa Faarisy kiongozi wa Madina baada kufungua Fursy.
Ameingia ‘Abdallah bin ‘Umar kwa babake akasema nimepewa elfu tatu na amepewa Usama elfu nne, akasema nimeshuhudia mambo asiyoshuhudia Usama. Akasema ‘Umar “Mzidishieni kwani yeye anapendwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuliko mimi, na Babake alikuwa akipendwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuliko mimi, kisha akawapa watu pesa kutokana na vyeo vyao, na kuhifadhi kwao Qur’an”
Ndugu Waislamu, hapana shaka ya kuwa neema ya udugu wa Kiislamu baina ya waumini na kupendana baina ya waja wa Mwenyezi Mungu ni katika neema kubwa juu ya umma huu. Na Mwenyezi Mungu Amewaamrisha waja wake kushikamana na udugu wa kiislamu, na kupendana.
Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى) وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ([آل عمران: 103]
{{Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane}}.
Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu ametulazimisha kupendana, na sura za kupendana ni kama zifuatazo:-
Kuwanusuru Waislamu na kuwasaidia nafsi, mali na ulimi. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى) : وَإِنِ اسْتَنْصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ( [الأنفال: 72]
{{Na watakapo kuombeni nusra, basi wasaideni kwa kuwanusuru ndugu zenu}}.
Kuwa na uchungu kwa anachokipata muumini kwa jambo la huzuni na kufurahi wanapofurahika. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Waumini kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni kama mwili mmoja].
Kuwanasihi waumini na kuwatakia kheri. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee kheri ndugu yake anachokipendelea nafsi yake].
Kuwaheshimu waumini na kuwanyenyekea, kutowatia aibu na kutowasengenya, Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَومٌ مِنْ قَوْمٍ) [الحجرات: 11]
{{Enyi mlio amini, Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao}}.
Kuwa na waumini wakati wa furaha na shida.
Kuwatembelea na kuwa pamoja nao amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mapenzi yangu yanastahiki kwa wenye kupendana kwa ajili yangu, na wenye kutembeleana kwa ajili yangu].
Kuheshimu haki ya waumini. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Asiuze Muislamu mauzo ya Muislamu mwenzake wala asipose posa ya mwenzake].
Kuwaombea waumini. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى: (وَاسْتَغْفِرْ لِذَنْبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ) [محمد: 19]
{{Naomba msamaha kwa madhambi yako, na uwaombe msamaha waumini wa kiume na waumini wa kike}}.
Inapaswa kutowapenda makafiri na kutojifananisha nao, na akaamrisha waja wake kuwahalifu makafiri kwa kila jambo (Ibada, ada, itikadi). Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Atakayejifananisha na watu basi ni katika wao]. Kupendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu humuinua mja sehemu ya juu. Hadithi ya watu wa saba watakao funikwa na kivuli cha Mwenyezi Mungu siku ambayo hakuna kivuli, mmoja wao; [Watu wawili waliopendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wamekusanyika kwa ajili yake na kutengana kwa ajili yake].
Imepokewa na Abu Huraira kuwa mtu ametoka kumtembelea mwenzake katika kijiji kingine basi Mwenyezi Mungu akamtuma Malaika, akamuulize Yule mtu anaenda wapi? Akasema anamkusudia mtu fulani, akasema Malaika je ana neema? Akasema namtembelea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, akasema Malaika basi mimi ni Malaika shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu anakupenda kwa kumpenda ndugu yako”
Imepokewa hadithi ya Mtume kuwa: [Imani thabiti ni kupendana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu].
Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Enyi watu sikieni na mtie akili, kwamba Mwenyezi Mungu ana waja si manabii wala sio mashuhadaa, wanatamaniwa na manabii na mashuhadaa kwa daraja waliyonao na ukaribu wao kwa Mwenyezi Mungu]. Hao ni watu kutoka maeneo tofauti na kabila tofauti tofauti, hawana kati yao ukaraba, wamependana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, watakalia makalio ya nuru siku ya Qiyama yaliyoandaliwa na Mwenyezi Mungu, na nyuso zao kuwa na nuru, na nguo zao kuwa na nuru, wanaogopa watu wala hawaogopi, hao ndio mawalii wa Mwenyezi Mungu hawana hofu wala huzuni”
Mwisho
Ndugu Waislamu, tabia njema na maadili mema ndio mizani ya sheria ya kupima kila jambo wakati ukitaka kuamiliana na jambo hilo. Vilevile, ni mizani ya kuamiliana na watu aina tofauti – Muislamu na asiyekuwa Muislamu. Muislamu ana haki zake juu yako. Na asiyekuwa Muislamu ana haki zake kulingana na misingi ya kisheria.
Tunamuomba Allah atuwafikishe tuweza kutekeleza haki za waja kama alivyo tuamrisha kupitia mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Ewe Mola wetu turuzuku mwisho mwema, na utupe hapa duniani mema na kesho akhera, Ewe Mola wetu usitupe chuki katika vifua vyetu, na utusamehe wewe ndio mwenye kusamehe.