islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUJIANDAA NA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI TUKUFU


13165
wasifu
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi mtukufu. Katika mwezi huu milango ya Pepo inafunguliwa na milango ya Moto inafungwa.Ni mwezi ulio bora kuliko miezi mingine. Katika mwezi huo, Mwenyezi Mungu Amewaneemesha waja Wake kwa kuwafungulia mlango wa matarajio kwa kuachwa huru na Moto. Mwenyezi Mungu, kila usiku miongoni mwa masiku ya Ramadhani, ana waachwa huru wajawake na Moto. Basi yapasa kwa Waumini wajitayarishe nayo na kujianda kupokeya kwa amali njema,wala sio kupokeya kwa masiya.
Khutba ya

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Ametuwekea misimu mbali mbali na kwa minaajili ya kuipatiliza misimu hiyo kwa kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kukufanya ibada, miongoni mwa misimu hiyo ni mwezi wa Ramadhani.

Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Misimu ya Twaa na Kuipaliza

Baada ya kumshukuru Allah. Mwenyezi Mungu mtakatifu ametuambia:

قال الله عز وجل: (شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآَنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَنْ كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ) [البقرة: 185]{{Mwezi wa Ramadhani ambao umeteremshwa Qur’an ndani yake ambayo ni ubainifu na uongofu kwa watu na upambanuzi. Mwenye kuushuhudia Mwezi wa Ramadhani miongoni mwenu na afunge na atakayekuwa mgonjwa ama akawa safarini (na akala katika mwezi wa Ramadhani) basi ni juu yake kufunga katika siku nyengine, Mwenyezi Mungu awatakia wepesi na wala hawatakii uzito na ili mukamilishe hesabu ya masiku na mumtukuze Mweyezi Mungu, hakika mukifanya hivyo mutakuwa ni wenye shukrani}}.

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, mwezi mtukufu wa Ramadhani umetukabili inatupasa tuupokee kwa kumcha Mwenyezi Mungu na kufanya twaa na ibada kwa wingi na kukaa mbali na maovu kama tunavyo jua ya kuwa malipo ya amali njema huongezeka na vile vile malipo ya amali mbaya. Na mwezi huu mtukufu mwanzo ni kumi la rehma na kumi la maghfira na mwisho ni kuachwa huru na moto. Kufunga mchana ni wajibu na kusimama kwa ibada usiku ni sunna yenye kukamilisha faradhi. Ukifunga kwa imani na kutarajia malipo utasamehewa madhambi yaliyotanguliia. Ukifanya ‘umra ni kama uliye hijji. Milango ya pepo hufunguliwa na ya moto hufungwa. Na saumu ni ibada ya pekee ambayo Mola amejihusishia mwenyewe kama alivyosema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika hadithi ya Bukhari aliyoipokea kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mwenyezi Mungu amesema [Amali zote za binaadamu ni zake ila saumu. Hakika ya saumu ni yangu na ni Mimi ndiye nitakaye ilipa na saumu ni kinga, ikiwa ni siku ya mmoja wenu kufunga basi asifanye machafu, wala asiseme maovu, basi atakapo tukanwa na yoyote au akataka kupigana naye basi amwambie mimi nimefunga. Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake harufu ya kinywa cha mmoja wenu ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, na mwenye kufunga ana furaha mbili, moja huipata akifungua saumu, na ya pili ni wakati akikutana na Mola wake].

Wakati wa kufunga Mwezi wa Ramadhani

Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi, kwani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amekataza kutangulia kufunga Ramadhani kwa siku moja ama mbili ila ikiwa mtu ana ada ya funga yake kama vile jumatatu na Alkhamisi, na haifai kufunga siku ya shaka, Amesema Ammar bin Yaasir “Mwenye kufunga siku ya shaka basi amemuasi Abal Qaasim, yaani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Na amepokea Bukhari kutoka kwa Ibnu ‘Umar ya kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema katika maana ya Aya: [Msifunge mpaka muuone mwezi wala msifunguwe mpaka muuone mwezi, na iwapo mtafinikwa na mawingu kamilisheni hesabu ya thalathini]. Na atakaye uona mwezi kwa yaqini na amjulishe kiongozi aliyewakilishwa wala asifiche.

Na utakapotangazwa mwezi katika vyombo vya habari, kuingia kwa Ramadhani fungeni na kutoka kwa Ramadhani fungueni, kwani kutangaza kwa kiongozi aliyewakilishwa ndio hukumu.

Kufunga Mwezi wa Ramadhani ni nguzo moja katika uislamu na mwenye kupinga huwa kafiri.

Kufunga ni nguzo iliothibiti katika Qur-ani na mwenye kupinga huwa amemkanusha Mungu na Mtume na maelewano ya Waislamu wote Allah atwambia:

 

قال الله تعالى) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ) [البقرة: 183]

{{Enyi mlio amini mmefaradhiwa swaumu kama walivyofaradhiwa waliotangulia}}. Na saumu ni wajibu kwa kila muislamu alio baleghe na akawa na akili na uwezo wa kufunga, na mwanamke asiyekuwa na hedhi. Kafiri si wajibu kufunga, lakini ataulizwa siku ya kiyama na akisilimu halazimishwi kulipa zilizopita ila akisilimu katikati ya huo mchana wa Ramadhani atalazimika akamilishe siku na mtoto mdogo si wajibu kufunga mpaka abaleghe lakini yafaa tuwafundishe kufunga kama walivyokuwa masahaba. Na kubaleghe kwa mtoto hujulikana kwa moja katika mambo matatu: Jambo la kwanza; ni kufikia miaka kumi na mitano. Jambo la pili; ni kutokwa na manii kwa kuota, ama jambo jingine. Jambo la tatu; ni kutokwa na nywele za kinena. Na mtoto wa kike huzidisha Jambo la nne nalo nikupatwa na hedhi. Mtoto akipatwa na mambo haya tuliyoyataja, humlazimu faradhi zote za Mwenyezi Mungu ikiwa ana akili.

Na mwendawazimu si wajibu kufunga wala faradhi yoyote nyingine. Na wala mwenye kushindwa kufunga kwa sababu ya utu zima ama ugonjwa ambao hautarajiwi kupona, itakuwa si lazima kufunga lakini atalisha maskini kila siku alioacha atalisha maskini mmoja, kila maskini robo ya pishi kwa pishi za Mtume na ni bora kumuongezea kitoweo.

Ni nini Hukumu ya Wenye Udhuru katika kufunga ?

Mgonjwa anayetarajiwa kupona, ikiwa saumu haimsumbui wala kumdhuru, haifai kula kama mtu huyo hana udhuru wowote. Na ikwa saumu inamsumbua lakini haimdhuru na inafaa afungue na ni karaha kufunga na ikiwa saumu itamdhuru ni haramu kufunga na popote atakapopoa itamlazimu ailipe saumu na akifa kabla ya kupona hana madhambi.

Na mwanamke mwenye mimba akiwa ni dhaifu ama mimba itamletea uzito akashindwa kufunga mwanamke huyo anaruhusiwa asifunge lakini akihisi ya kuwa na uwezo wa kufunga, atafunga hata ikiwa ni kabla ya kujifungua na itakapokuwa haiwezekani atasubiri baada ya kujifungua na kutwahirika na nifasi. Na mwanamke mwenye kunyonyesha akiogopea kupunguka maziwa atakula kisha atalipa.

Na msafiri akikusudia kukimbia saumu haifai ni lazima afunge. Na ikiwa hakukusudia kukimbia kufunga basi ana hiari ya kufunga na kutofunga. Na ikiwa kufunga na kutofunga ni sawa basi ni bora afunge.

Na ikiwa safari itamsumbua ni karaha kufunga iwapo mashaka yatazidi na ni haramu kufunga. Kwani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alitoka kwenda Makka mwaka wa fat-hi na huku amefunga akaambiwa kuna watu wameshindwa kufunga na wanakusubiri wewe utakavyofanya. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaitisha maji akanywa na watu wanamwangalia kisha na watu wakanywa, kisha akaambiwa kuna watu hawakufungua akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hayo ni maasi].

Na safari ni ya aina yoyote ile, kama madereva wa malori wakati wowote wanapoacha miji yao wanaruhusiwa kufungua kama vile wanavyoruhusiwa kupunguza swala za rakaa nne na kuzikusanya swala mbili mbili ikiwa mtu amesafiri katikati ya mchana ni vizuri akamilishe saumu ya siku ile ya kwanza ya safari.

Na haifai kufunga kwa mwenye hedhi na nifasi na wala haiswihi. Wakati wakitwahirika na hedhi ni lazima wafunge hata kama hawajaoga kisha watalipa siku walizokula.

Kuhimiza kusimama Usiku wa Ramadhani na kuwanasihi Maimamu kuwa na makini katika Swala bila kuangalia wingi au uchache wa Rakaa

Enyi Waislamu, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amehimiza kusimama kufanya ibada katika masiku ya Ramadhanii. Na mtu akiendelea na imamu kuswali mpaka akamaliza huandikiwa thawabu za mtu aliyesimama usiku kucha.

Na ni juu ya maimamu kumcha Mwenyezi Mungu katika kuswalisha tarawehe. Inafaa awachunge wanaomfuata asiwaendeshe mbio bila ya utulivu katika kusimama, kurukuu na kusujudu. Kwani Mwenyezi Mungu Amesema (Subhaanahu wa Taala) katika mafhum ya Aya:

قال الله تعالى) : (لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا) [هود: 7]

{{Ili apate kuwaonja walio na amali nzuri zaidi (sio walio na amali za haraka zaidi)}}. Na Mtume alikuwa ni mwenye kupenda kheri zaidi na ni kielelezo chema lakini hakuzidisha zaidi ya rakaa kumi na moja sio katika Ramadhanii wala masiku mengine. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) aliswali na jamaa katika Ramadhani kisha akaacha kwa kuogopea isifaradhishwe.

Na iliyo swahihi kutoka kwa Amirul muuminiina ‘Umar ibnul Khatwb ni kuwa alimuamrisha ‘Ubai ibn Ka’ab na Tamimi Daar waswalishe watu kwa rakaa kumi na moja na hii ndio idadi aliodumu nayo Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na akafuata khalifa muongofu ‘Umar Ibnul khatwab ndio bora zaidi, na ikiwa mtu atazidisha kwa mapenzi yake sio kufuata sunna hapingwi lakini asifanye haraka kama wanavyofanya maimamu wabaya.

Mungu atuafikie kupaliza nyakati za twaa na atuhifadhi na maovu na atuongoze njia iliyonyooka na atuepushe na njia ya motoni na atufanye wenye kufunga Ramadhani na wenye kusimama usiku kwa ibada kwa imani na kutarajia malipo na thawabu za Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyyezi Mungu ni Mpaji na ni Mkarimu.

Namaliza maneno yangu kwa kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha na kuwaombea Waislamu wote msamaha kutokana na madhambi yote.

Faida za Kufunga:

Miongoni mwa faida ni kuivunja nafsi, kwani shibe ya maji na chakula na kuvaana na wanawake inapelekea kughafilika.

Faida nyingine ni moyo kukaa faragha kwa kumfikiria Mwenyezi Mungu na kuleta dhikri, kwani tumbo likiwa tupu husababisha moyo kunawirika.

Na faida nyingine ni kwa mtu tajiri hujua neema ya Mola juu yake. Kwa sababu ya kujinyima kwa muda fulani na hupelekea kumkumbuka ndugu yake aliyenyimwa neema ile moja kwa moja humsikitikia mwenzake maskini.

Na saumu hufanya mapitio ya damu kuwa membamba ambayo ndio mapitio ya shetani, kwani shetani anatembea katika mwili kama inavyotembea damu basi Mtume amesema “Fungeni mapito ya shetani kwa njaa.”

Saumu ya Mja haiwezi kutimia ila akiepuka yaliyo haramishwa katika hali zote.

Kwani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amesema [Ambaye haachi maneno ya uongo na kutumia uongo, Mwenyezi Mungu hana haja aache chakula chake na kinywaji chake]. Na watu wema ilikuwa wakifunga hukaa Msikitini ili kuepukana na kusengenya.

Khutba ya pili

Makundi ya Wenye kufunga

Kuna makundi mawili ya wenye kufunga:

Wanaofunga kutarajia pepo.

Wanaofunga kuacha dunia na kuelekea kwa Allah (Subhanahu wa Taala).

Imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). katika swahihi mbili akisema [Hakika katika pepo kuna mlango unaoitwa Rayyan, haingii yoyote isipokuwa wenye kufunga]. Na katika riwaya nyingine: [wakiingia utafungwa]. Hiyo ndiyo tabaka la kwanza, ambao wanatarajia pepo, huyu amefanya na Mola atamlipa. Ama tabaka la pili ni ambao wanafunga na wanaepukana na dunia, huhifadhi kichwa na kilochokusanya (macho, masikio, na mdomo) na huhifadhi tumbo, na hukumbuka mauti na kuoza baada ya kufa. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema :

قال الله تعالى) : مَنْ كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ اللَّهِ فَإِنَّ أَجَلَ اللَّهِ لَآَتٍ( {{Mwenye kutarajia [العنكبوت: 5]kukutana na Mwenyezi Mungu, hakika ajali ya Mungu inakuja}}.

Na Mwenyezi Mungu amesema katika maana ya Hadithi al-Qudsi: [Saumu ni yangu na mimi ndiye mwenye kuilipa].

Ubora wa Mwezi wa Ramadhani

Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال الله تعالى) : شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآَنُ) [البقرة: 185]

{{Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa Qur-ani ndani yake}}. Na Ibnu ‘Abbas (Radhiya Llahu ‘anhu) amesema Qur-ani iliteremshwa kwa mara moja kutoka Lauhul mahfuudh mpaka Baitul ‘izza katika usiku wa cheo. Na ushahidi ni kuwa Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قوله تعالى : (إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ) [القدر: 1].

{{Hakika yetu sisi tumeiteremsha Qur’an katika usiku wa cheo}}. Na maswahaba walikuwa wakisimama usiku mpaka karibia na alfajiri. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ulikuwa ukarimu wake ukizidi katika mwezi wa Ramadhani na hiyo ni sababu ya kukaa sana na Jibril kwa kumsomea Qur-ani na kumhimiza katika tabia njema.

Faida za kuwa Mkarimu katika Mwezi wa Ramadhani.

Ya kwanza ni utukufu wa zile zama na kuongezeka malipo ya amali

Ya pili ni kuwasaidia wenye kufunga na wenye kufanya ibada katika ibada zao.

Ya tatu ni kuwa katika Ramadhani Allah anawakirimu waja wake kwa rehema na maghfira kuwaacha huru na moto haswa katika Lailatul Qadri kwa Allah anawarehemu waja wake wenye sikitiko zaidi.

Ya nne, kuchanganya baina ya saumu na sadaka ni katika mambo yenye kumtia mtu peponi.

Ya tano, kufunga pamoja na kutoa sadaka ni mambo yanayofuta madhambi zaidi na kuepushwa na moto wa jahanamu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Saumu ni kinga].

Ya sita hakika ya saumu hakuna budi kutapatikana kasoro au upungufu, basi sadaka itaziba kasoro hiyo au upungufu huo na ndio ikawajibishwa kutoa Zakatul fitri.

Ya saba, Imam Shafi amesema inapendeza zaidi kwa mtu kufanya wingi wa kutoa katika mwezi wa Ramadhani ili kumwiga Mtume na watu kuhitajia maslahi yao na watu kushughulika na ibada na kuwacha kufanya kazi. Ewe Mola tukubalie funga yetu na kisimamo chetu. Ewe Mola msamehe aliyekufa na aliye hai kati yetu na mdogo wetu na mkubwa wetu na mume na mke na aliyeko na asiyekuweko miongoni mwetu.

Mwisho

Enyi ndugu Waislamu, tujipinde katika mwezi wa Ramadhani kwani tusipo fanya hivyo tutakuwa mbali na rehma za Allah (Subhaanahu wa Taala) na kama tulivyobainisha ya kuwa twaewza tukafunga njaa iwapo hatutaepukana na makatazo ya Allah katika hali ya kufunga.





Vitambulisho: